9 Yesu aliondoka hapo, na alipokuwa anakwenda zake, alimwona mtu mmoja aitwaye Mathayo, ameketi katika ofisi ya ushuru. Basi, Yesu akamwambia, “Nifuate.” Naye Mathayo akainuka, akamfuata.
10 Yesu alipokuwa nyumbani ameketi kula chakula, watozaushuru wengi na wahalifu walikuja wakaketi pamoja naye na wanafunzi wake.
11 Mafarisayo walipoona hayo, wakawaambia wanafunzi wake, “Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watozaushuru na wenye dhambi?”
12 Yesu aliwasikia, akasema, “Watu wenye afya hawahitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa.
13 Basi, kajifunzeni maana ya maneno haya: ‘Nataka huruma, wala si tambiko.’ Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi.”
14 Kisha wanafunzi wa Yohane Mbatizaji walimwendea Yesu, wakamwuliza, “Sisi na Mafarisayo hufunga mara nyingi; mbona wanafunzi wako hawafungi?”
15 Yesu akawajibu, “Je, walioalikwa harusini hutakiwa kuomboleza wakati bwana arusi yupo pamoja nao? La, hasha! Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga.