8 Wote waishio duniani watamwabudu isipokuwa tu wale ambao majina yao yameandikwa tangu mwanzo wa ulimwengu katika kitabu cha uhai cha Mwanakondoo aliyechinjwa.
9 Aliye na masikio, na asikie!
10 Aliyepangiwa kuchukuliwa mateka lazima atatekwa;wa kuuawa kwa upanga atauawa kwa upanga.Hivyo, watu wa Mungu na wawe na uvumilivu na imani.
11 Kisha, nikamwona mnyama mwingine anatoka ardhini. Alikuwa na pembe mbili kama pembe za kondoo, na aliongea kama joka.
12 Alikuwa na mamlaka kamili kutoka kwa yule mnyama wa kwanza, na akautumia uwezo huo mbele ya huyo mnyama. Akailazimisha dunia yote na wote waliomo humo kumwabudu huyo mnyama wa kwanza ambaye alikuwa na jeraha la kifo lililokuwa limepona.
13 Basi, huyu mnyama wa pili akafanya miujiza mikubwa hata akasababisha moto kutoka mbinguni ushuke duniani mbele ya watu.
14 Aliwapotosha wakazi wa dunia kwa miujiza hiyo aliyojaliwa kutenda mbele ya mnyama wa kwanza. Aliwaambia wakazi wa dunia watengeneze sanamu kwa heshima ya yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini akaishi tena.