1 Baada ya hayo, nilimwona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa na uwezo mkuu, na dunia ikamulikwa na mng'ao wake.
2 Basi, akapaza sauti kwa nguvu akisema, “Umeanguka; Babuloni mkuu umeanguka! Sasa umekuwa makao ya mashetani na pepo wachafu; umekuwa makao ya ndege wachafu na wa kuchukiza mno.
3 Maana mataifa yote yalileweshwa kwa divai kali ya uzinzi wake, nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi naye. Nao wafanyabiashara wa dunia wametajirika kutokana na anasa zake zisizo na kipimo.”
4 Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema,“Watu wangu, ondokeni kwake,ili msishirikiane naye katika dhambi zake,msije mkaipata adhabu yake.
5 Kwa maana dhambi zake zimekuwa nyingi mno,zimerundikana mpaka mbinguni,na Mungu ameyakumbuka maovu yake.
6 Mtendeeni kama alivyowatendea nyinyi;mlipeni mara mbili kwa yale aliyoyatenda.Mchanganyieni kikombeni mwake kinywaji kikali maradufu.