1 Kisha, nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu ile ya kwanza na dunia ile ya kwanza vilikuwa vimetoweka, nayo bahari pia haikuwako tena.
2 Nikaona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni. Ulikuwa umetayarishwa vizuri kama bibi arusi aliyepambwa tayari kukutana na mumewe.
3 Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka katika kiti cha enzi ikisema, “Tazama! Maskani ya Mungu kati ya watu. Atakaa kati yao, nao watakuwa watu wake, naye atakuwa Mungu wao.
4 Yeye atayafuta machozi yao yote; maana kifo hakitakuwako tena, wala uchungu, wala kilio, wala maumivu; maana ile hali ya kale imepita!”