5 Kisha yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi akasema, “Tazama, nafanya yote mapya.” Tena akaniambia, “Andika jambo hili, maana maneno haya ni ya kuaminika na ya kweli!”
6 Kisha akaniambia, “Yametimia! Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Aliye na kiu nitampa kinywaji cha bure kutoka katika chemchemi ya maji ya uhai.
7 Mshindi yeyote atapokea hicho, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.
8 Lakini watu waoga, wasioamini, wapotovu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, na waongo wote, mahali pao patakuwa ndani ya lile ziwa linalowaka moto na madini ya kiberiti; hicho ndicho kifo cha pili.”
9 Kisha mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba yaliyokuwa yamejaa mabaa saba ya mwisho, akaja na kuniambia, “Njoo! Nami nitakuonesha bibi arusi, mkewe Mwanakondoo!”
10 Basi, Roho akanikumba, naye malaika akanipeleka juu ya mlima mrefu sana. Akanionesha mji mtakatifu, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni,
11 uking'aa kwa utukufu wa Mungu. Mwangaza wake ulikuwa kama wa jiwe la thamani kubwa kama yaspi, angavu kama kioo.