13 “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!
14 “Kwa malaika wa kanisa la Laodikea andika hivi:“Mimi niitwaye Amina, shahidi mwaminifu na wa kweli, ambaye ni chanzo cha viumbe vyote alivyoumba Mungu nasema hivi.
15 Nayajua mambo yako yote! Najua kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungekuwa kimojawapo: Baridi au moto.
16 Basi, kwa kuwa hali yako ni vuguvugu, si baridi wala si moto, nitakutapika!
17 Wewe unajisema, ‘Mimi ni tajiri; ninajitosheleza, sina haja ya kitu chochote;’ kumbe, hujui kwamba wewe ni mnyonge, unahitaji kuhurumiwa, maskini, kipofu tena uko uchi!
18 Nakushauri ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto upate kuwa tajiri kweli. Tena afadhali ununue pia vazi jeupe, uvae na kufunika aibu ya uchi wako. Nunua pia mafuta ukapake machoni pako upate kuona.
19 Mimi ndiye mwenye kumwonya na kumrudi yeyote ninayempenda. Kwa hiyo uwe na bidii na kutubu.