22 Kwa hiyo tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu na imani timilifu, kwa mioyo iliyotakaswa kutokana na dhamiri mbaya, na kwa miili iliyosafishwa kwa maji safi.
23 Tuzingatie kabisa tumaini letu tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu.
24 Tujitahidi kushughulikiana kwa ajili ya kuongezeana bidii ya kupendana na kutenda mema.
25 Tusiache ile desturi ya kukutana pamoja, kama vile wengine wanavyofanya. Bali tunapaswa kusaidiana kwani, kama mwonavyo, siku ile ya Bwana inakaribia.
26 Maana, tukiendelea kutenda dhambi makusudi baada ya kufahamu ukweli, hakuna tambiko iwezayo kutolewa tena kwa ajili ya kuondoa dhambi.
27 Linalobaki ni kungojea tu kwa hofu hukumu ya Mungu na moto mkali utakaowaangamiza wote wanaompinga.
28 Mtu yeyote asiyetii sheria ya Mose, huuawa bila huruma kukiwa na ushahidi wa watu wawili au watatu.