7 Kwa imani Noa alionywa na Mungu juu ya mambo ya baadaye ambayo hayakuwa yameonekana bado. Alimtii Mungu, akajenga ile safina ambamo aliokolewa yeye pamoja na jamaa yake. Kutokana na hayo ulimwengu ulihukumiwa, naye Noa akapokea uadilifu unaotokana na imani.
8 Kwa imani Abrahamu alimtii Mungu alipoitwa aende katika nchi ambayo Mungu angempa iwe yake. Ingawa hakujua alikokuwa anakwenda, Abrahamu alihama.
9 Kwa imani aliishi kama mgeni katika nchi aliyoahidiwa na Mungu. Aliishi huko katika hema kama walivyoishi Isaka na Yakobo, ambao pia walishiriki ahadi ileile.
10 Maana Abrahamu alikuwa akingojea mji wenye misingi imara, mji ambao Mungu mwenyewe ndiye fundi aliyeubuni na kuujenga.
11 Kwa imani hata Sara aliamini kwamba Mungu hutimiza ahadi zake, kwa hiyo akajaliwa kuchukua mimba ingawaje alikuwa amepita umri.
12 Kwa hiyo, kutoka katika mtu huyo mmoja, Abrahamu, ambaye alikuwa kama amekufa, walitokea watu wengi wasiohesabika kama vile nyota za mbinguni na mchanga wa pwani.
13 Watu hawa wote walikufa wakiwa na imani. Walikufa kabla ya kupokea mambo ambayo Mungu alikuwa ameahidi, lakini kwa mbali waliyaona, wakashangilia, na kukiri wazi kwamba wao walikuwa wageni na wakimbizi duniani.