2 Ujumbe ule waliopewa wazee wetu na malaika ulioneshwa kuwa kweli, hata mtu yeyote ambaye hakuufuata au hakuutii aliadhibiwa kama alivyostahili.
3 Basi, sisi tutaokokaje kama hatuujali wokovu mkuu kama huu? Kwanza Bwana mwenyewe aliutangaza wokovu huu, na wale waliomsikia walituthibitishia kwamba ni kweli.
4 Mungu pia aliongeza hapo ushahidi wake kwa kufanya kila namna ya miujiza na maajabu, na kwa kuwagawia watu vipaji vya Roho Mtakatifu kadiri ya mapenzi yake.
5 Mungu hakuwaweka malaika wautawale ulimwengu ujao, yaani ulimwengu ule tunaoongea habari zake.
6 Tena yasemwa mahali fulani katika Maandiko:“Mtu ni nini, hata umfikirie;mwanadamu ni nini hata umjali?
7 Ulimfanya tu kidogo kuwa chini ya malaika;umemvika taji ya utukufu na heshima,
8 ukaweka kila kitu chini ya miguu yake.”Yasemwa kwamba Mungu alimweka mtu kuwa mtawala wa vitu vyote, yaani bila kuacha hata kimoja. Hata hivyo, hatuoni bado mtu akivitawala vitu vyote sasa.