1 Yesu alipokwisha sema hayo, alikwenda ngambo ya kijito Kedroni, pamoja na wanafunzi wake. Mahali hapo palikuwa na bustani, naye Yesu akaingia humo pamoja na wanafunzi wake.
2 Yuda, aliyemsaliti Yesu, alipajua mahali hapo kwani mara nyingi Yesu alikutana na wanafunzi wake huko.
3 Basi, Yuda alichukua kikosi cha askari na walinzi kutoka kwa makuhani wakuu na Mafarisayo, akaja nao bustanini wakiwa na taa, mienge na silaha.
4 Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawauliza, “Mnamtafuta nani?”
5 Nao wakamjibu, “Yesu Mnazareti!” Yesu akawaambia, “Mimi ndiye.” Msaliti Yuda alikuwa amesimama hapo pamoja nao.
6 Basi, Yesu alipowaambia: “Mimi ndiye,” wakarudi nyuma, wakaanguka chini.