16 Shupimu na Hosa waliangukiwa na kura ya kulinda lango la magharibi kwenye lango la Shalekethi kwenye barabara ya juu. Ulinzi ulifanywa kwa zamu.
17 Kila siku upande wa mashariki kulikuwa na mabawabu sita, kaskazini wanne, na kusini wanne, pia kwenye ghala kuliwekwa mabawabu wawiliwawili.
18 Kwenye banda zuri lililokuwa upande wa magharibi, kulikuwa na mabawabu wanne barabarani, na wawili kwenye banda lenyewe.
19 Haya ndiyo makundi ya mabawabu miongoni mwa ukoo wa Kora na wazawa wa Merari waliofanya kazi ya ubawabu.
20 Miongoni mwa Walawi, Ahiya alihusika na uangalizi wa hazina ya nyumba ya Mungu, na hazina ya vitu vilivyowekwa wakfu.
21 Ladani, mmoja wa ukoo wa Gershoni, alikuwa babu wa baadhi ya jamaa, miongoni mwao ikiwamo jamaa ya mwanawe Yehieli.
22 Wana wengine wawili wa Ladani, Zethamu na Yoeli, walikuwa watunzaji wa hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.