1 Mambo Ya Nyakati 16 BHN

1 Kisha waliliingiza sanduku la Mungu, na kuliweka ndani ya hema ambayo Daudi alikuwa ameitayarisha. Halafu wakatoa tambiko za kuteketezwa na za amani mbele ya Mungu.

2 Daudi alipomaliza kutoa tambiko hizo za kuteketezwa na za amani, aliwabariki watu katika jina la Mwenyezi-Mungu,

3 na akawagawia Waisraeli wote, wanaume kwa wanawake, kila mmoja akapewa mkate, kipande cha nyama na mkate wa zabibu.

4 Zaidi ya hayo, Daudi aliwateua baadhi ya Walawi wawe wahudumu wa sanduku la Mwenyezi-Mungu, wamtukuze, wamtolee shukrani na wamsifu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.

5 Alimchagua Asafu kuwa kiongozi wao, akisaidiwa na Zekaria. Yeieli, Shemiramothi, Yehieli, Metithia, Eliabu, Benaya, Obed-edomu na Yehieli, aliwachagua wawe wapiga vinanda na vinubi. Asafu alipiga matoazi,

6 nao makuhani Benania na Yaharieli, walichaguliwa wawe wakipiga tarumbeta mfululizo mbele ya sanduku la agano la Mungu.

7 Basi, hiyo ikawa siku ambayo kwa mara ya kwanza, Daudi alimpa Asafu na ndugu zake Walawi wajibu wa kumwimbia Mwenyezi-Mungu nyimbo za shukrani.

Wimbo wa Sifa

8 Mpeni shukrani Mwenyezi-Mungu,tangazeni ukuu wake,yajulisheni mataifa mambo aliyoyatenda!

9 Mshangilieni, mwimbieni Mungu sifa;simulieni matendo yake ya ajabu!

10 Jisifieni jina lake takatifu;wenye kumcha Mwenyezi-Mungu na wafurahi.

11 Mwendeeni Mwenyezi-Mungu mwenye nguvu;mwendeeni Mwenyezi-Mungu daima.

12 Kumbukeni matendo ya ajabu aliyotenda,maajabu yake na hukumu alizotoa,

13 enyi wazawa wa Abrahamu, mtumishi wake,enyi wazawa wa Yakobo, wateule wake.

14 Yeye Mwenyezi-Mungu, ndiye Mungu wetu;hukumu zake zina nguvu duniani kote.

15 Yeye hulishika agano lake milele,hutimiza ahadi zake kwa vizazi elfu.

16 Hushika agano alilofanya na Abrahamu,na ahadi aliyomwapia Isaka.

17 Alimthibitishia Yakobo ahadi yake,akamhakikishia agano hilo la milele.

18 Alisema: “Nitawapeni nchi ya Kanaani,nayo itakuwa mali yenu wenyewe.”

19 Idadi yenu ilikuwa ndogo,mlikuwa wachache na wageni katika nchi ya Kanaani,

20 mkitangatanga toka taifa hadi taifa,kutoka nchi moja hadi nchi nyingine,

21 Mungu hakumruhusu mtu yeyote awadhulumu;kwa ajili yao aliwaonya wafalme:

22 “Msiwaguse wateule wangu;msiwadhuru manabii wangu!”

23 Mwimbieni Mwenyezi-Mungu, ulimwengu wote.Tangazeni kila siku matendo yake ya wokovu.

24 Yatangazieni mataifa utukufu wake,waambieni watu wote matendo yake ya ajabu.

25 Maana Mwenyezi-Mungu ni mkuu, anasifika sanaanastahili kuheshimiwa kuliko miungu yote.

26 Miungu yote ya mataifa mengine si kitu;lakini Mwenyezi-Mungu aliziumba mbingu.

27 Utukufu na fahari vyamzunguka,nguvu na furaha vyajaza hekalu lake.

28 Mpeni Mwenyezi-Mungu, heshima enyi jamii zote za watu,naam, kirini utukufu na nguvu yake.

29 Mpeni Mwenyezi-Mungu heshima ya utukufu wa jina lake;leteni tambiko na kuingia nyumbani mwake.Mwabuduni Mwenyezi-Mungu patakatifuni pake.

30 Ee dunia yote; tetemeka mbele yake!Ameuweka ulimwengu imara, hautatikisika.

31 Furahini enyi mbingu na dunia!Yaambieni mataifa, “Mwenyezi-Mungu anatawala!”

32 Bahari na ivume, pamoja na vyote vilivyomo!Furahini enyi mashamba na vyote vilivyomo!

33 Ndipo miti yote msituni itaimba kwa furahambele ya Mwenyezi-Mungu anayekujanaam, anayekuja kuihukumu dunia.

34 Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema,kwa maana fadhili zake zadumu milele!

35 Mwambieni Mwenyezi-Mungu:Utuokoe, ee Mungu wa wokovu wetu,utukusanye pamoja na kutuokoa kutoka kwa mataifa,tupate kulisifu jina lako takatifu,kuona fahari juu ya sifa zako.

36 Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli,tangu milele na hata milele!Kisha watu wote wakasema, “Amina!” Pia wakamsifu Mwenyezi-Mungu.

Ibada huko Yerusalemu na Gibeoni

37 Hivyo, mfalme Daudi akawaacha Asafu na nduguze Walawi mahali walipoliweka sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, kwa ajili ya huduma zinazotakiwa mbele ya sanduku kila siku.

38 Obed-edomu, mwana wa Yeduthuni, pamoja na wenzake sitini na wanane waliwasaidia. Obed-edomu mwana wa Yeduthuni na Hosa walikuwa walinzi wa malango.

39 Mfalme Daudi akawaweka kuhani Sadoki na makuhani wenzake kuwa wahudumu wa hema ya Mwenyezi-Mungu iliyokuwa mahali pa kuabudu huko Gibeoni

40 ili kutolea Mwenyezi-Mungu sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya sadaka za kuteketezwa daima asubuhi na jioni, kulingana na yote yaliyoandikwa katika sheria ya Mwenyezi-Mungu aliyowaamuru Waisraeli.

41 Pamoja nao walikuwa Hemani na Yeduthuni na wale wote waliochaguliwa, waliotajwa majina yao, ili kumshukuru Mwenyezi-Mungu kwa kuwa fadhili zake ni za milele.

42 Hemani na Yeduthuni walikuwa na tarumbeta na matoazi kwa ajili ya muziki na ala za muziki kwa ajili ya nyimbo takatifu. Wana wa Yeduthuni walichaguliwa kuyalinda malango.

43 Kisha, kila mtu aliondoka kwenda nyumbani kwake; naye Daudi akaenda nyumbani kwake kuibariki jamaa yake.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29