1 Mambo Ya Nyakati 26 BHN

Walinzi wa hekalu

1 Haya ndiyo makundi ya Walawi waliofanya kazi za ubawabu. Kutoka katika ukoo wa Kora, alikuwa Meshelemia mwana wa Kore wa jamaa ya Asafu.

2 Yeye alikuwa na wana saba: Zekaria mzaliwa wake wa kwanza, Yediaeli wa pili, Zebadia wa tatu, Yathnieli wa nne,

3 Elamu wa tano, Yohanani wa sita na Eliehoenai wa saba.

4 Pia kulikuwa na Obed-edomu, ambaye Mungu alimbariki kwa kumpa wana wanane: Shemaya mzaliwa wake wa kwanza, Yehozabadi wa pili, Yoa wa tatu, Sakari wa nne, Nethaneli wa tano,

5 Amieli wa sita, Isakari wa saba na Peulethai wa nane.

6 Naye mwanawe Shemaya alipata wana waliokuwa na mamlaka juu ya jamaa ya baba yao, kwa sababu walikuwa wanaume wenye uwezo mkubwa.

7 Shemaya, mzaliwa wa kwanza wa Obed-edomu, alikuwa na wana sita: Othni, Refaeli, Obedi, Elizabadi, nduguze walikuwa mashujaa, Elihu na Semakia.

8 Hao wote wana wa Obed-edomu; wao na wana wao na ndugu zao, walikuwa watu hodari wawezao huo utumishi. Wazawa wote wa Obed-edomu walikuwa sitini na wawili.

9 Naye Meshelemia alikuwa na wana na nduguze; watu wenye uwezo kumi na wanne.

10 Hosa mmojawapo wa wana wa Merari alikuwa na wana wanne: Shimri (aliyefanywa kiongozi na baba yake hata ingawa hakuwa mzaliwa wa kwanza),

11 Hilkia wa pili, Tebalia wa tatu na Zekaria wa nne. Wana wote wa Hosa pamoja na nduguze walikuwa kumi na watatu.

12 Mabawabu hao waligawanyika katika makundi kulingana na jamaa zao, nao pia walipangiwa kazi kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu kama wale Walawi wengine.

13 Kila jamaa, bila kujali wingi, ilipiga kura kuchagua lango watakalosimamia.

14 Kura ya kuchagua wa kulinda lango la mashariki ilimwangukia Shelemia. Walipiga kura pia kwa ajili ya mwanawe Zekaria, aliyekuwa mshauri mwenye busara, ikamwangukia kura ya lango la kaskazini.

15 Obed-edomu aliangukiwa na kura ya lango la kusini, na ya wanawe, ghala.

16 Shupimu na Hosa waliangukiwa na kura ya kulinda lango la magharibi kwenye lango la Shalekethi kwenye barabara ya juu. Ulinzi ulifanywa kwa zamu.

17 Kila siku upande wa mashariki kulikuwa na mabawabu sita, kaskazini wanne, na kusini wanne, pia kwenye ghala kuliwekwa mabawabu wawiliwawili.

18 Kwenye banda zuri lililokuwa upande wa magharibi, kulikuwa na mabawabu wanne barabarani, na wawili kwenye banda lenyewe.

19 Haya ndiyo makundi ya mabawabu miongoni mwa ukoo wa Kora na wazawa wa Merari waliofanya kazi ya ubawabu.

Kazi nyingine za hekaluni

20 Miongoni mwa Walawi, Ahiya alihusika na uangalizi wa hazina ya nyumba ya Mungu, na hazina ya vitu vilivyowekwa wakfu.

21 Ladani, mmoja wa ukoo wa Gershoni, alikuwa babu wa baadhi ya jamaa, miongoni mwao ikiwamo jamaa ya mwanawe Yehieli.

22 Wana wengine wawili wa Ladani, Zethamu na Yoeli, walikuwa watunzaji wa hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

23 Pia kazi ziligawanywa kwa watu wa koo za Wasiria, Waishari, Wahebroni na Wauzieli.

24 Shebueli, mwana wa Gershoni, mwana wa Mose, alikuwa ofisa mkuu wa hazina hizo.

25 Na ndugu yake, alikuwa Eliezeri, aliyekuwa baba yake Rehabia, aliyemzaa Yeshaya, aliyemzaa Yoramu, aliyemzaa Zikri, aliyemzaa Shelomithi.

26 Shelomithi na ndugu zake, ndio waliokuwa waangalizi wa hazina zote za vitu vilivyowekwa wakfu na mfalme Daudi, na viongozi wa jamaa, maofisa wa maelfu na mamia na majemadari wa jeshi.

27 Waliweka wakfu sehemu ya nyara walizoteka vitani kwa ajili ya matengenezo ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

28 Pia, vitu vyote vilivyowekwa wakfu na Samueli, mwonaji, na Shauli mwana wa Kishi, na Abneri, na Yoabu mwana wa Seruya, vilikuwa chini ya uangalizi wa Shelomithi na nduguze.

Kazi za Walawi wengine

29 Miongoni mwa Waishari, Kenania na wanawe walipewa kazi za utawala kama maofisa na waamuzi, kwa ajili ya Waisraeli.

30 Miongoni mwa Wahebroni, Hashabia na nduguze 1,700, wote watu mashujaa walipewa wajibu wa kusimamia sehemu za Israeli zilizokuwa upande wa magharibi wa mto Yordani. Walisimamia kazi yote ya Mwenyezi-Mungu na kazi za mfalme Daudi.

31 Miongoni mwa Wahebroni, Yeria alikuwa kiongozi wa koo na jamaa zote, na katika mwaka wa arubaini wa utawala wa mfalme Daudi, uchunguzi ulifanywa, na wanaume wenye uwezo mkubwa walipatikana huko Yezeri katika Gileadi.

32 Mfalme Daudi alimteua Yeriya na ndugu zake 2,700, mashujaa na viongozi wa koo, kusimamia mambo yote yaliyohusu Mungu na mfalme Daudi katika sehemu za Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, zilizokuwa mashariki ya mto Yordani.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29