1 Mfalme Daudi akawakusanya huko Yerusalemu wakuu wote wa Israeli: Wa makabila, majemadari na vikosi waliomtumikia mfalme, makamanda wa maelfu, makamanda wa mamia, wasimamizi wa mali zote na ng'ombe wote wa mfalme, na wanawe pamoja na maofisa wa ikulu, mashujaa na askari wote mashuhuri.
2 Ndipo mfalme Daudi akasimama akasemana kusema: “Enyi ndugu zangu na watu wangu, nisikilizeni. Nilikusudia moyoni mwangu kujenga nyumba kwa ajili ya sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, kiti cha kuwekea miguu yake Mungu wetu; na nilifanya maandalizi ya kujenga.
3 Lakini Mungu alinikataza, kwa sababu mimi ni mtu wa vita na nimekwisha mwaga damu nyingi.
4 Lakini Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli alinichagua mimi miongoni mwa jamaa ya baba yangu kuwa mfalme wa Israeli milele. Alilichagua kabila la Yuda liongoze; na kutokana na kabila hilo, aliichagua jamaa ya baba yangu, na miongoni mwa wana wa baba yangu, alipendezwa nami na kuniweka niwe mfalme wa Israeli yote.