18 na kiasi cha dhahabu safi ya kutengenezea madhabahu ya kufukizia ubani. Alimpa pia mfano wake wa gari la dhahabu la viumbe wenye mabawa waliyotandaza mabawa na kulifunika sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu.
19 Hayo yote, mfalme Daudi aliyaweka wazi kwa maandishi aliyopewa na Mwenyezi-Mungu. Kazi yote itendeke kulingana na ramani hiyo.
20 Kisha, mfalme Daudi akamwambia Solomoni mwanawe, “Uwe imara na hodari, uifanye kazi hii. Usiogope wala kuwa na wasiwasi. Mungu, Mwenyezi-Mungu ambaye ni Mungu wangu, yu pamoja nawe. Hatakuacha bali atakuwa nawe hata itakapomalizika kazi yote inayohitajika kufanyiwa nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
21 Makuhani na Walawi wamekwisha pangiwa kazi watakazofanya katika nyumba ya Mungu. Wafanyakazi wenye ujuzi wa kila aina watakuwa tayari kabisa kukusaidia, na watu wote pamoja na viongozi wao watakuwa chini ya amri yako.”