26 kwa maana wale walinzi wakuu wanne, ambao walikuwa Walawi, walikuwa na wajibu wa kusimamia vyumba na hazina ya nyumba ya Mungu.
27 Wao waliishi karibu na nyumba ya Mungu kwa sababu ilikuwa ni wajibu wao kuyalinda na kuyafungua malango yake kila siku asubuhi.
28 Baadhi ya Walawi walisimamia vyombo vilivyotumika wakati wa ibada. Walihitajika kuvihesabu wakati vilipotolewa na wakati viliporudishwa.
29 Wengine walichaguliwa kuvisimamia vifaa vya hekalu, na vyombo vyote vitakatifu, na unga safi, divai, mafuta ya zeituni, ubani na manukato.
30 Lakini kazi ya kutayarisha manukato ilifanywa na makuhani.
31 Metithia, mmoja wa Walawi aliyekuwa mzaliwa wa kwanza wa Shalumu, wa ukoo wa Kora, alisimamia utengenezaji wa tambiko ya mikate myembamba.
32 Nao ndugu zao wengine wa ukoo wa Kohathi walikuwa na wajibu wa kutayarisha mikate ya wonyesho kwa ajili ya hekalu kila Sabato.