13 Samueli akamjibu Shauli, “Umefanya kipumbavu. Hukutii aliyokuamuru Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. Kama ungetii, Mwenyezi-Mungu angeudumisha milele ufalme wako juu ya Israeli.
14 Lakini sasa ufalme wako hautadumu kwa kuwa amri aliyokuamuru Mwenyezi-Mungu hukuitii. Mwenyezi-Mungu amejitafutia mtu mwingine ambaye atamtii kwa moyo wote, na huyo ndiye ambaye amemteua kuwa mtawala juu ya watu wake.”
15 Samueli akaondoka kutoka Gilgali na kwenda huko Gibea katika nchi ya Benyamini.Shauli alipowahesabu watu waliokuwa pamoja naye, aliona wako watu 600 tu.
16 Shauli na Yonathani mwanawe pamoja na watu waliokuwa pamoja nao, walikaa huko Gibea katika nchi ya Benyamini na Wafilisti walipiga kambi huko Mikmashi.
17 Wafilisti walitoka kwenye kambi yao kwenda kuwashambulia wakiwa wako katika vikosi vitatu. Kikosi kimoja kilielekea Ofra katika nchi ya Shuali.
18 Kikosi kingine kilielekea Beth-horoni, na kikosi kingine kikageukia njia ielekeayo bonde la Seboimu, kuelekea jangwani.
19 Wakati huo hapakuwepo na mhunzi yeyote katika nchi nzima ya Israeli, kwani Wafilisti walikusudia kuwazuia Waebrania wasije wakajitengenezea mapanga au mikuki.