1 Kisha mfalme Nahashi wa Waamoni, alikwenda na kuuzingira mji wa Yabesh-gileadi. Wakazi wa mji wa Yabesh-gileadi wakamwambia Nahashi, “Fanya mapatano nasi, nasi tutakutumikia.”
2 Lakini akawaambia, “Nitafanya mapatano nanyi kwa sharti moja kwamba nitamngoa kila mmoja wenu jicho lake la kulia; hivyo nitawaaibisha Waisraeli wote.”
3 Wazee wa Yabeshi wakamwambia, “Tupe muda wa siku saba ili tuwatume wajumbe katika nchi yote ya Israeli. Kama hakuna mtu yeyote wa kutuokoa, tutajisalimisha wenyewe kwako.”
4 Wale wajumbe walipofika mjini Gibea, alikoishi Shauli, wakaeleza habari hizo na watu wote wakaanza kulia kwa sauti.
5 Sasa, Shauli alikuwa anatoka shambani akiwa na fahali wake, akauliza, “Watu wana nini? Kwa nini wanalia?” Wakamwambia habari waliyoleta wajumbe kutoka Yabeshi.
6 Mara, Shauli aliposikia maneno hayo, roho ya Mungu ikamjia kwa nguvu, naye akawaka hasira kali.
7 Akachukua fahali wawili akawakatakata vipandevipande, akatuma wajumbe wavipitishe kila mahali nchini Israeli wakisema, “Mtu yeyote ambaye hatamfuata Shauli na Samueli vitani, fahali wake watafanywa hivyo.” Hofu ikawaaingia Waisraeli kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu angeweza kufanya. Kwa hiyo, wote walitoka kwa pamoja.
8 Shauli alipowapanga Waisraeli huko Bezeki akawa na watu 300,000 kutoka Israeli na 30,000 kutoka Yuda.
9 Wakawaambia wale wajumbe waliorudi kutoka Yabeshi, “Waambieni hivi wakazi wa Yabesh-gileadi: Kesho, wakati jua linapokuwa kali, mtakuwa mmekombolewa.” Watu wa Yabeshi walipopata habari hizo walifurahi sana.
10 Hivyo, wakamkejeli Nahashi wakimwambia, “Kesho tutajisalimisha kwako, nawe utatutendea lolote unaloona ni jema.”
11 Kesho yake, Shauli aliwagawa watu katika vikosi vitatu. Wakati wa zamu ya asubuhi, wakaingia kwenye kambi ya adui, na kuwashambulia Waamoni. Kufikia adhuhuri adui wengi walikuwa wamekatiliwa mbali. Wale walionusurika walitawanyika ovyo, hata kusiwe kikundi chochote cha watu wawili pamoja.
12 Ndipo Waisraeli wakamwambia Samueli, “Wako wapi wale watu waliosema Shauli asiwe mfalme juu yetu? Tuletee watu hao, nasi tutawaulia mbali.”
13 Lakini Shauli akawaambia, “Hakuna mtu yeyote atakayeuawa leo, kwa kuwa katika siku hii, Mwenyezi-Mungu ameikomboa Israeli.”
14 Samueli akawaambia, “Twendeni wote Gilgali na kwa mara nyingine tutamtangaza Shauli kuwa mfalme.”
15 Watu wote wakaenda Gilgali, na walipofika huko, wakamtawaza Shauli kuwa mfalme mbele ya Mwenyezi-Mungu. Wakamtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za amani hapo. Na Shauli pamoja na watu wote wa Israeli wakafurahi sana.