1 Samueli 4 BHN

Sanduku la agano linatekwa

1 Wakati huo, Wafilisti walikutana pamoja, wapigane na Waisraeli. Waisraeli walipiga kambi yao huko Ebenezeri, na Wafilisti wakapiga kambi yao huko Afeka.

2 Wafilisti waliwashambulia Waisraeli, na baada ya mapigano makali, Waisraeli walishindwa. Waisraeli 4,000 waliuawa kwenye uwanja wa mapambano.

3 Wanajeshi walionusurika walipowasili kambini, wazee wa Israeli walisema, “Kwa nini Mwenyezi-Mungu amewaacha Wafilisti watushinde leo? Twendeni tukalilete sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu kutoka Shilo, ili aweze kwenda nasi vitani na kutuokoa kutoka na zetu.”

4 Hivyo, walituma watumishi huko Shilo, nao wakalileta sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu wa majeshi ambaye anakaa kifalme juu ya viumbe wenye mabawa. Wale watoto wawili wa kiume wa Eli, Hofni na Finehasi walikuja pamoja na lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu.

5 Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilipofika kambini Waisraeli wote walishangilia kwa furaha, hata nchi yote ikatikisika.

6 Wafilisti waliposikia sauti hiyo ya furaha walisema “Kelele hizo zote kambini mwa Waebrania zina maana gani?” Walipojua kwamba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilikuwa limewasili kambini mwa Waisraeli,

7 Wafilisti waliogopa; wakasema, “Bila shaka, miungu imewasili kambini mwao! Ole wetu! Jambo kama hili halijawahi kutokea.

8 Ole wetu! Ni nani atakayeweza kutuokoa kutokana na miungu hiyo yenye nguvu? Hiyo ni miungu iliyowaua Wamisri kwa kila aina ya mapigo jangwani.

9 Sasa, enyi Wafilisti, jipeni moyo. Muwe, hodari msije mkawa watumwa wa Waebrania kama wao walivyokuwa watumwa wetu. Muwe hodari kama wanaume na kupigana.”

10 Wafilisti walipiga vita, na Waisraeli walishindwa na kukimbia kila mtu nyumbani kwake. Siku hiyo kulikuwa na mauaji makubwa kwani askari wa miguu 30,000 wa Israeli waliuawa.

11 Sanduku la agano la Mungu lilitekwa, na wale watoto wawili wa kiume wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa.

Kifo cha Eli

12 Siku hiyohiyo, mtu mmoja wa kabila la Benyamini alikimbia kutoka mstari wa mbele wa mapigano mpaka Shilo huku mavazi yake yakiwa yamechanika na akiwa na mavumbi kichwani.

13 Eli, akiwa na wasiwasi moyoni kuhusu sanduku la Mungu, alikuwa ameketi kwenye kiti chake, kando ya barabara akiangalia. Yule mtu alipowasili mjini na kueleza habari hizo, mji mzima ulilia kwa sauti.

14 Eli aliposikia sauti ya kilio, akauliza, “Kelele hizo ni za nini?” Yule mtu akaenda haraka kwa Eli ili kumpa habari hizo.

15 Wakati huo, Eli alikuwa na umri wa miaka tisini na nane na macho yake yalikuwa yamepofuka.

16 Yule mtu akamwambia Eli, “Mimi nimetoka vitani sasa hivi; nimekimbia kutoka vitani leo.” Eli akamwuliza, “Mwanangu, mambo yalikuwaje huko?”

17 Yule aliyeleta habari akasema, “Waisraeli wamewakimbia Wafilisti. Kumekuwa na mauaji makubwa miongoni mwa Waisraeli. Zaidi ya yote, wanao wote wawili, Hofni na Finehasi, wameuawa, na sanduku la agano la Mungu limetekwa.”

18 Huyo mtu alipotaja tu sanduku la Mungu, Eli alianguka chali kutoka kwenye kiti chake kando ya lango. Eli alipoanguka hivyo, shingo yake ilivunjika kwani alikuwa mzee na mnene, naye akafariki. Eli alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka arubaini.

Kifo cha mjane wa Finehasi

19 Tena ilitokea kwamba, mkwewe Eli, yaani mke wa Finehasi, wakati huo alikuwa mjamzito, na muda wake wa kujifungua ulikuwa umekaribia. Aliposikia kwamba sanduku la agano la Mungu limetekwa na kwamba baba mkwe wake, hata na mumewe wamefariki, mara moja alipata utungu, na kujifungua.

20 Basi, alipokuwa anakufa, wanawake waliokuwa wanamsaidia walimwambia, “Usiogope, maana umejifungua mtoto wa kiume.” Lakini yeye hakujibu neno, wala hakuwasikiliza.

21 Naye akamwita mtoto wake Ikabodi, akimaanisha, “Utukufu wa Mungu umeondoka Israeli,” akiwa na maana kwamba sanduku la agano lilikuwa limetekwa, tena baba mkwe wake na mumewe, wote walifariki.

22 Akasema, “Utukufu wa Mungu umeondoka Israeli kwani sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu limetekwa.”

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29 30 31