1 Samueli 31 BHN

Kifo cha Shauli na wanawe

1 Basi, Wafilisti walipigana vita dhidi ya Waisraeli; nao Waisraeli walikimbia mbele ya Wafilisti, na kuuawa katika mlima wa Gilboa.

2 Lakini Wafilisti wakamzingira Shauli na wanawe, kisha wakawaua Yonathani, Abinadabu na Malki-shua, wana wa Shauli.

3 Vita vilikuwa vikali sana dhidi ya Shauli. Wapiga mishale walipomwona walimjeruhi vibaya.

4 Ndipo Shauli alipomwambia mtu aliyembebea silaha, “Chomoa upanga wako unichome nife, ili watu hawa wasiotahiriwa wasije wakanichoma upanga na kunidhihaki.” Lakini huyo aliyembebea silaha hakuthubutu kwa sababu aliogopa sana. Hivyo, Shauli alichukua upanga wake mwenyewe, na kuuangukia.

5 Halafu yule aliyembebea silaha alipoona kuwa Shauli amekufa, naye pia aliuangukia upanga wake, akafa pamoja na Shauli.

6 Hivyo ndivyo Shauli alivyokufa, na wanawe watatu, pia na mtu aliyembebea silaha pamoja na watu wake wote katika siku hiyohiyo moja.

7 Nao Waisraeli waliokuwa upande wa pili wa bonde, na wengine waliokuwa upande wa mashariki wa mto Yordani walipoona kuwa Waisraeli wamekimbia, naye Shauli na wanawe wamekufa, waliihama miji yao, wakakimbia. Wafilisti wakaenda na kukaa katika miji hiyo.

8 Kesho yake, Wafilisti walipokwenda kuwateka nyara hao waliouawa walizikuta maiti za Shauli na wanawe mlimani Gilboa.

9 Walikata kichwa cha Shauli na kumvua silaha zake; halafu waliwatuma wajumbe katika nchi yao yote ya Filistia kutangaza habari njema nyumbani mwa sanamu zao na kwa watu.

10 Zile silaha zake waliziweka nyumbani mwa Maashtarothi; kisha wakautundika mwili wake kwenye ukuta wa mji wa Beth-sheani.

11 Lakini wakazi wa mji wa Yabesh-gileadi waliposikia Wafilisti walivyomtendea Shauli,

12 mashujaa wote waliondoka, wakasafiri usiku kucha, wakaondoa mwili wa Shauli na miili ya wanawe kutoka ukuta wa Beth-sheani; wakaja nayo mpaka Yabeshi na kuiteketeza huko.

13 Baadaye, wakaichukua mifupa yao na kuizika chini ya mkwaju huko Yabeshi; nao wakafunga kwa muda wa siku saba.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29 30 31