1 Halafu Hana aliomba na kusema:“Namshangilia Mwenyezi-Mungu moyoni mwangu.Namtukuza Mwenyezi-Mungu aliye nguvu yangu.Nawacheka adui zangu;maana naufurahia ushindi wangu.
2 “Hakuna aliye mtakatifu kama Mwenyezi-Mungu;hakuna yeyote aliye kama yeye;hakuna aliye mwamba kama Mungu wetu.
3 Acheni kujisifu,acheni kusema ufidhuli.Maana ajuaye ni Mwenyezi-Mungu.Yeye huyapima matendo yote.
4 Pinde za wenye nguvu zimevunjika.Lakini wadhaifu wanaendelea kupata nguvu.
5 Wale ambao zamani walikuwa na chakula tele,sasa wanaajiriwa ili wapate chakula.Lakini waliokuwa na njaa,sasa hawana njaa tena.Mwanamke tasa amejifungua watoto saba.Lakini mama mwenye watoto wengi,sasa ameachwa bila mtoto.
6 Mwenyezi-Mungu huua na hufufua;yeye huwashusha chini kuzimunaye huwarudisha tena.
7 Mwenyezi-Mungu huwafanya baadhi wawe maskini,na baadhi wawe matajiri.Wengine huwashusha,na wengine huwakweza.
8 Huwainua maskini toka mavumbini;huwanyanyua wahitaji toka majivuni,akawaketisha pamoja na wakuu,na kuwarithisha viti vya heshima.Maana, minara ya dunia ni ya Mwenyezi-Mungu;yeye ameisimika dunia juu ya minara yake.
9 “Maisha ya waaminifu wake huyalinda,lakini maisha ya waovu huyakatilia mbali gizani.Maana, binadamu hapati ushindi kwa nguvu zake.
10 Maadui wa Mwenyezi-Mungu watavunjwa vipandevipande;atanguruma dhidi yao kama radi mbinguni.Mwenyezi-Mungu ataihukumu dunia yote;atampa nguvu mfalme wakeataukuza uwezo wa mteule wake.”
11 Kisha, Elkana akarudi nyumbani Rama. Lakini mtoto Samueli akabaki Shilo kumtumikia Mwenyezi-Mungu chini ya uongozi wa kuhani Eli.
12 Watoto wa kiume wa Eli walikuwa walaghai sana. Hawakumjali Mwenyezi-Mungu
13 wala juu ya vitu ambavyo watu walipaswa kuwapa makuhani. Kila mara mtu alipokuwa anatolea tambiko yake, mtumishi wa kuhani alikuja na uma wenye meno matatu; na wakati nyama ikiwa bado inachemka,
14 huyo mtumishi aliuchomeka uma huo ndani ya chungu, nyama yoyote iliyotolewa humo na uma huo, ilikuwa mali ya kuhani. Waisraeli wote waliokwenda Shilo kutolea tambiko zao walitendewa hivyo.
15 Zaidi ya hayo, hata kabla mafuta hayajachomwa, mtumishi wa kuhani huja na kumwambia yule mtu anayetoa tambiko, “Mtolee kuhani nyama ya kubanika maana yeye hatapokea nyama yako iliyochemshwa, bali iliyo mbichi.”
16 Na kama mtu huyo akimjibu, “Ngojea kwanza nichome mafuta halafu utachukua kiasi chochote unachotaka,” hapo huyo mtumishi wa kuhani humjibu, “La, ni lazima unipe sasa hivi. La sivyo, nitaichukua kwa nguvu.”
17 Dhambi hii ya vijana hao wa Eli ilikuwa kubwa sana mbele ya Mwenyezi-Mungu. Maana, vijana hao walidharau matoleo ya Mwenyezi-Mungu.
18 Wakati huo, kijana Samueli aliendelea kumtumikia Mwenyezi-Mungu, akiwa amevaa kizibao cha kitani.
19 Kila mwaka mama yake alimfumia vazi dogo, na kumpelekea alipokuwa akienda na mumewe kutolea tambiko ya kila mwaka.
20 Eli aliwabariki Elkana na mkewe, akisema, “Mwenyezi-Mungu na akupe wewe Elkana watoto wengine kwa mwanamke huyu ili wachukue mahali pa yule uliyempa Mwenyezi-Mungu.” Kisha wao hurudi nyumbani.
21 Mwenyezi-Mungu alimhurumia Hana naye akajaliwa kupata watoto wa kiume watatu na mabinti wawili. Mtoto Samueli akaendelea kukua mbele ya Mwenyezi-Mungu.
22 Wakati huo Eli alikuwa mzee sana. Aliposikia yote ambayo watoto wake wa kiume walikuwa wanawatendea Waisraeli, jinsi walivyokuwa wanalala na wanawake waliokuwa wanahudumu kwenye mlango wa hema la mkutano,
23 aliwauliza, “Kwa nini mnafanya mambo haya? Nasikia kutoka kwa watu wote juu ya maovu mnayoyafanya.
24 Msifanye hivyo wanangu kwa sababu mambo hayo ninayoyasikia kutoka kwa watu wa Mwenyezi-Mungu ni mabaya.
25 Mtu akimkosea mwenzake, anaweza kuombewa kwa Mungu, ili Mungu amsamehe. Lakini mtu akimkosea Mwenyezi-Mungu nani awezaye kumwombea msamaha?” Lakini watoto hao hawakumsikiliza baba yao, kwani Mwenyezi-Mungu alikwisha kata shauri kuwaua.
26 Mtoto Samueli aliendelea kukua, akazidi kupendwa na Mwenyezi-Mungu na watu.
27 Siku moja, mtu wa Mungu alimwendea Eli, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu amesema hivi: ‘Nilijijulisha kwa jamaa ya Aroni, wazee wako, walipokuwa watumwa wa Farao nchini Misri.
28 Kati ya makabila yote ya Israeli nilimchagua Aroni na jamaa yake kuwa makuhani wangu, wanitumikie madhabahuni, wafukize ubani na kuvaa kizibao mbele yangu. Nikaipatia jamaa ya mzee wako tambiko zangu ambazo Waisraeli walinitolea kwa moto.
29 Kwa nini basi, umezionea wivu tambiko na sadaka nilizowaamuru watu waniletee? Wewe umewastahi watoto wako kuliko mimi kwa kujinenepesha nyinyi wenyewe kwa kula sehemu nzurinzuri za sadaka ambazo watu wangu wa Israeli hunitolea!’
30 Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anatamka hivi, ‘Niliahidi kwamba jamaa yako na jamaa ya wazee wako mtakuja mbele yangu kunitumikia milele;’ lakini sasa Mwenyezi-Mungu anakutangazia hivi, ‘Jambo hilo liwe mbali nami.’ Nitawaheshimu wale wanaoniheshimu, na wale wanaonidharau, nitawadharau.
31 Angalia siku zaja ambapo nitawaua vijana wote wa kiume katika jamaa yako na katika ukoo wako, hata hakutakuwa na mwanamume yeyote atakayeishi awe mzee.
32 Utakuwa na wasiwasi na utawaonea wenzio kijicho kwa zile baraka zote ambazo nitawapa watu wengine wa Israeli, lakini hakuna mtu katika jamaa yako atakayeishi na kuwa mzee.
33 Mtu wako ambaye sitamkatilia mbali kutoka madhabahu yangu atakuwa amenusurika ili nimpofushe macho yake, naye atakufa moyo na wazawa wako watauawa kikatili.
34 Na litakalowapata watoto wako wawili wa kiume, Hofni na Finehasi, ni hili: Wote wawili watakufa siku moja. Hii itakuwa ni ishara kwako.
35 Kisha, nitajiinulia kuhani mwingine mwaminifu atakayefanya kulingana na yale yaliyomo moyoni na akilini mwangu. Nitamjengea ukoo imara, naye atahudumu daima mbele ya mfalme wangu.
36 Yeyote atakayebakia katika jamaa yako atamwendea kuhani huyo na kumwomba kipande cha fedha au mkate, na kumwambia, ‘Niweke, nakuomba, kwenye nafasi mojawapo ya kuhani ili niweze, angalau, kupata kipande cha mkate.’”