1 Samueli alimwambia Shauli, “Mwenyezi-Mungu alinituma kukupaka mafuta uwe mfalme wa watu wake wa Israeli. Sasa sikiliza maneno ya Mwenyezi-Mungu.
2 Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Nitawaadhibu Waamaleki kwa sababu waliwapiga Waisraeli walipokuwa wanatoka Misri.
3 Sasa, nenda ukawashambulie na kuangamiza vitu vyote walivyo navyo. Usiwaache hai, ila uwaue wote: Wanaume kwa wanawake, watoto wachanga na wanyonyao, ng'ombe, kondoo, ngamia na punda.’”
4 Shauli akaliita jeshi lake, akalikagua huko Telaimu. Kulikuwa na askari wa miguu 200,000 kutoka Israeli na 10,000 kutoka Yuda.