1 Sasa, Wafilisti walikusanya majeshi yao huko Soko, mji ulioko katika Yuda, tayari kwa vita. Walipiga kambi katika sehemu moja iitwayo Efes-damimu kati ya Soko na Azeka.
2 Shauli pamoja na Waisraeli walikusanyika, na kupiga kambi katika bonde la Ela. Wakajipanga tayari kupigana na Wafilisti.
3 Wafilisti walisimama mlimani upande mmoja na Waisraeli walisimama mlimani upande mwingine, katikati yao kulikuwa na bonde.
4 Kutoka kwenye kambi ya Wafilisti, alijitokeza shujaa mmoja aitwaye Goliathi, mwenyeji wa mji wa Gathi. Urefu wake ulikaribia mita tatu.
5 Kichwani alivaa kofia ya shaba, na deraya ya shaba kifuani yenye uzito wa kilo 57.
6 Miguu yake pia ilikuwa na kinga ya shaba na mabegani pake alibeba mkuki wa shaba.