30 Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anatamka hivi, ‘Niliahidi kwamba jamaa yako na jamaa ya wazee wako mtakuja mbele yangu kunitumikia milele;’ lakini sasa Mwenyezi-Mungu anakutangazia hivi, ‘Jambo hilo liwe mbali nami.’ Nitawaheshimu wale wanaoniheshimu, na wale wanaonidharau, nitawadharau.
31 Angalia siku zaja ambapo nitawaua vijana wote wa kiume katika jamaa yako na katika ukoo wako, hata hakutakuwa na mwanamume yeyote atakayeishi awe mzee.
32 Utakuwa na wasiwasi na utawaonea wenzio kijicho kwa zile baraka zote ambazo nitawapa watu wengine wa Israeli, lakini hakuna mtu katika jamaa yako atakayeishi na kuwa mzee.
33 Mtu wako ambaye sitamkatilia mbali kutoka madhabahu yangu atakuwa amenusurika ili nimpofushe macho yake, naye atakufa moyo na wazawa wako watauawa kikatili.
34 Na litakalowapata watoto wako wawili wa kiume, Hofni na Finehasi, ni hili: Wote wawili watakufa siku moja. Hii itakuwa ni ishara kwako.
35 Kisha, nitajiinulia kuhani mwingine mwaminifu atakayefanya kulingana na yale yaliyomo moyoni na akilini mwangu. Nitamjengea ukoo imara, naye atahudumu daima mbele ya mfalme wangu.
36 Yeyote atakayebakia katika jamaa yako atamwendea kuhani huyo na kumwomba kipande cha fedha au mkate, na kumwambia, ‘Niweke, nakuomba, kwenye nafasi mojawapo ya kuhani ili niweze, angalau, kupata kipande cha mkate.’”