4 Yonathani akamwambia, “Lolote utakalosema nitakutendea.”
5 Daudi akamwambia, “Kesho ni sherehe za mwezi mwandamo, nami natazamiwa kuwapo mezani kula pamoja na mfalme. Lakini niache, nikajifiche huko shambani hadi siku ya tatu jioni.
6 Baba yako akinikosa mezani kwa chakula, akauliza habari zangu, basi mwambie, ‘Daudi amenisihi nimpe ruhusa ili aende mjini kwake Bethlehemu, kuhudhuria tambiko ya kila mwaka pamoja na jamaa yake’.
7 Ikiwa ataona hilo ni sawa, basi, ujue kuwa mambo yangu, mimi mtumishi wako, yako sawa. La sivyo, kusudi lake juu yangu ni baya.
8 Hivyo nifanyie kwa hisani yako kwani umefanya agano takatifu nami, mimi mtumishi wako, mbele ya Mwenyezi-Mungu. Lakini, kama nimefanya kosa basi, na uniue wewe mwenyewe; kwa nini unipeleke kwa baba yako ili aniue?”
9 Yonathani akamjibu, “Wazo hilo na liwe mbali nawe. Hakika, kama ningejua kuwa baba yangu amekusudia mabaya juu yako nisingekuficha.”
10 Daudi akauliza, “Nitajuaje ikiwa baba yako atakujibu kwa ukali?”