8 Walituma wajumbe na kuwakusanya wakuu wote wa Wafilisti na kuwauliza, “Je, tutafanya nini na sanduku hili la Mungu wa Israeli?” Wakuu wao wakajibu, “Sanduku hilo la Mungu wa Israeli lipelekeni Gathi.” Basi, wakalipeleka kwenye mji wa Gathi.
9 Lakini baada ya kulipeleka huko Gathi, Mwenyezi-Mungu akauadhibu mji huo, akisababisha hofu kuu mjini, na akawapiga wanaume wa mji huo, vijana kwa wazee, kwa kuwaletea majipu.
10 Hivyo, wakalipeleka sanduku hilo la Mungu kwenye mji wa Ekroni. Lakini sanduku hilo la Mungu lilipofika huko, watu wa mji huo walipiga kelele, “Wametuletea sanduku la Mungu wa Israeli ili kutuua sisi na watu wetu.”
11 Kisha wakatuma ujumbe na kukusanya wakuu wa Wafilisti na kuwaambia, “Lirudisheni sanduku la Mungu wa Israeli mahali pake, ili lisituue sisi pamoja na watu wetu.” Walifanya hivyo kwa sababu kulikuwa na hofu kubwa katika mji mzima kwa sababu Mungu alikuwa anawaadhibu vikali.
12 Nao wale ambao hawakufa walipatwa na majipu hata kilio cha mji kilifika mbinguni.