11 Samueli aliwaambia, “Hivi ndivyo mfalme wenu atakayewatawala atakavyowatendea: Watoto wenu wa kiume atawafanya wawe waendeshaji wa magari yake, na wengine kuwa wapandafarasi wake, na wengine watapiga mbio mbele ya magari yake.
12 Atajichagulia wengine wawe makamanda wa vikosi vyake vya maelfu na wengine wawe makamanda wa vikosi vya watu hamsinihamsini. Atawafanya wengine wamlimie mashamba yake na kuvuna mazao yake. Atawafanya wengine pia wamtengenezee zana za vita, na wengine wamtengenezee vipuli vya magari yake.
13 Binti zenu atawachukua kuwa watengenezaji marashi, wengine wapishi na wengine waokaji mikate.
14 Atayachukua mashamba yenu mazuri, mashamba ya mizeituni, na mashamba ya mizabibu na kuwapa watumishi wake.
15 Atachukua sehemu ya kumi ya nafaka zenu na ya zabibu zenu na kuwapa maofisa wake na watumishi wake.
16 Atachukua watumishi wenu wa kiume na wa kike na ng'ombe wenu wazuri na punda wenu wazuri kabisa na kuwafanya wamfanyie kazi zake.
17 Atachukua sehemu ya kumi ya kondoo wenu. Na nyinyi wenyewe mtakuwa watumwa wake.