1 Basi, Rehoboamu akaenda Shekemu, ambako Waisraeli wote walikuwa wamekusanyika ili kumtawaza awe mfalme.
2 Naye Yeroboamu mwana wa Nebati alipopata habari kuhusu tendo hilo (wakati huo alikuwa bado anaishi Misri alikokwenda alipomkimbia Solomoni) alitoka Misri.
3 Lakini Waisraeli walituma ujumbe na kumwita. Kisha, yeye pamoja na Waisraeli wote walimwendea Rehoboamu na kumwambia,
4 “Baba yako alitutwika mzigo mzito. Basi, utupunguzie mzigo huo, nasi tutakutumikia.”
5 Rehoboamu akawajibu, “Rudini kwangu baada ya siku tatu.” Basi wakaondoka.
6 Baadaye, Rehoboamu alitaka kujua maoni ya wazee ambao walikuwa washauri wa Solomoni, baba yake, alipokuwa angali hai, akawauliza, “Je, mnanishauri niwape jibu gani watu hawa?”
7 Wazee hao wakamjibu, “Ukiwahurumia watu hawa, ukiwafurahisha na kusema nao maneno mazuri, hapo watakuwa watumishi wako daima.”