8 Lakini Rehoboamu alipuuza shauri la wazee na badala yake akashauriana na vijana wa rika lake ambao walikuwa washauri wake.
9 Basi, akawauliza, “Nyinyi mnatoa shauri gani ili tuweze kuwajibu watu hawa walioniambia, ‘Punguza mzigo ambao baba yako alitutwika?’”
10 Hao vijana wakamjibu, “Watu hao waliokuambia ‘Baba yako alitutwika mzigo mzito, lakini wewe utupunguzie,’ wewe waambie hivi: ‘Kidole changu kidogo cha mwisho ni kinene zaidi kuliko kiuno cha baba yangu.
11 Mzigo wa baba yangu ulikuwa mzito, lakini wangu utakuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba.’”
12 Basi katika siku ya tatu Yeroboamu pamoja na watu wote wakarudi kwa Rehoboamu kama alivyokuwa amewaagiza.
13 Naye mfalme Rehoboamu akawajibu kwa ukali, akapuuza shauri la wazee,
14 na kufuata shauri la vijana wenzake. Basi akasema, “Baba yangu aliwatwika mzigo mzito, lakini mimi nitaufanya kuwa mzito zaidi. Baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, lakini mimi nitawapiga kwa mijeledi yenye miiba”