12 Alipojinyenyekesha, Mwenyezi-Mungu aliacha kumghadhibikia na hakumwangamiza kabisa. Zaidi ya hayo, hali ya nchi ya Yuda ilikuwa nzuri.
13 Hivyo mfalme Rehoboamu alijiimarisha zaidi katika Yerusalemu, akaitawala Yuda. Alikuwa na umri wa miaka arubaini na mmoja alipoanza kutawala Yuda. Naye alitawala kwa muda wa miaka kumi na saba katika Yerusalemu, mji ambao Mwenyezi-Mungu aliuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli aabudiwe humo. Mama yake Rehoboamu aliitwa Naama, kutoka Amoni.
14 Rehoboamu alitenda maovu, kwa maana hakunuia kumtafuta Mwenyezi-Mungu kwa moyo.
15 Matendo yote ya mfalme Rehoboamu ya mwanzo mpaka ya mwisho na rekodi ya ukoo yameandikwa katika kitabu cha Kumbukumbu za nabii Shemaya, na Kumbukumbu za Ido Mwonaji. Wakati huu wote, kulikuwa na vita vya mfululizo kati ya Rehoboamu na Yeroboamu.
16 Hatimaye Rehoboamu alifariki na kuzikwa katika mji wa Daudi, na Abiya mwanawe, akatawala mahali pake.