1 Roho ya Mungu ilimjia Azaria mwana wa Odedi,
2 naye akatoka kwenda kumlaki mfalme Asa, akamwambia, “Nisikilize, ee mfalme Asa na watu wote wa Yuda na Benyamini! Mwenyezi-Mungu yu pamoja nanyi, ikiwa mtakuwa pamoja naye. Mkimtafuta, mtampata, lakini mkimwacha naye atawaacha.
3 Kwa muda mrefu sasa, Waisraeli wameishi bila Mungu wa kweli, wala makuhani wa kuwafundisha, na bila sheria.
4 Lakini walipopatwa na shida, walimgeukia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, wakamtafuta, wakampata.
5 Zamani hizo, hakuna mtu aliyeweza kuingia wala kutoka kwa usalama kwa sababu hapakuwa na amani; ghasia nyingi mno ziliwasumbua wananchi wa kila nchi.
6 Kulijaa mafarakano mengi, taifa moja lilipigana na taifa lingine na mji mmoja ulipigana na mji mwingine, kwa sababu Mungu aliwafadhaisha kwa taabu za kila aina.
7 Lakini nyinyi jipeni moyo, wala msilegee kwa maana mtapata tuzo kwa kazi mfanyayo.”