1 Naye Yehoshafati mwanawe alitawala mahali pa baba yake Asa, akajiimarisha dhidi ya Israeli.
2 Aliweka majeshi katika miji yote ya Yuda yenye ngome, na katika maeneo mengine ya Yuda, na katika miji ya Efraimu ambayo Asa baba yake aliiteka akaweka askari walinzi.
3 Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Yehoshafati kwa sababu alifuata njia za awali za baba yake, na wala hakumwabudu Baali.
4 Yeye alimtafuta Mungu wa baba yake na kuzitii amri zake, wala hakufuata matendo ya watu wa Israeli.
5 Mwenyezi-Mungu, aliuimarisha ufalme wa Yuda mikononi mwa Yehoshafati, nao watu wote wakamletea zawadi, akatajirika sana na kuheshimika.
6 Alipenda sana moyoni kumtumikia Mwenyezi-Mungu, na zaidi ya hayo, alipaharibu mahali pote pa kuabudia miungu mingine na sanamu za Ashera, mungu wa kike, nchini Yuda.
7 Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wake, Yehoshafati aliwatuma maofisa wafuatao wakafundishe katika miji ya Yuda: Ben-haili, Obadia, Zekaria, Nethaneli na Mikaya.