11 Hata wale manabii wengine wakatabiri vivyo hivyo wakasema, “Nenda ukaushambulie Ramoth-gileadi, Mwenyezi-Mungu atautia mikononi mwako.”
12 Wakati huo, yule mjumbe aliyetumwa kwa Mikaya alimwambia, “Manabii wengine wote kwa pamoja wamemtabiria mfalme ushindi; tafadhali nawe pia ufanye kama wao, umtabirie mema.”
13 Lakini Mikaya akamjibu, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo, kile atakachoniambia Mungu wangu, ndicho nitakachosema.”
14 Basi, Mikaya alipofika mbele ya mfalme, mfalme akamwuliza, “Je, twende kupigana vitani huko Ramoth-gileadi au nisiende?” Mikaya akajibu, “Nenda ushinde; Mwenyezi-Mungu atawatia mikononi mwako.”
15 Lakini mfalme akamwambia, “Nitakuapisha mara ngapi kwamba kila unaposema nami kwa jina la Mwenyezi-Mungu, ni lazima uniambie ukweli mtupu?”
16 Naye Mikaya akasema, “Niliwaona watu wote wa Israeli wametawanyika milimani kama kondoo wasio na mchungaji. Naye Mwenyezi-Mungu akasema, ‘Watu hawa hawana kiongozi; waache warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.’”
17 Hapo mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia, kamwe hatatabiri jema juu yangu, ila mabaya tu?”