1 Mfalme Solomoni alikata shauri kujenga nyumba ambamo Mwenyezi-Mungu ataabudiwa, na pia kujijengea yeye mwenyewe jumba la kifalme.
2 Alipanga wanaume 70,000 wawe wachukuzi wa mizigo, 80,000 wawe wachonga mawe milimani na wengine 3,600 wawe wasimamizi wao.
3 Kisha, Solomoni akatuma ujumbe kwa Hiramu, mfalme wa Tiro, akamwambia, “Nitendee na mimi kama ulivyomtendea baba yangu Daudi, ulipompelekea mierezi ya kujengea ikulu.
4 Tazama, karibu nianze kujenga nyumba ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu. Nitaiweka wakfu, nayo itakuwa mahali pa kufukiza ubani wa harufu nzuri mbele yake, na mahali pa mikate ya kuwekwa mbele yake daima, na tambiko za kuteketezwa asubuhi na jioni na pia siku za Sabato, mwezi mwandamo, na sikukuu nyinginezo za Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kama alivyoiagiza Israeli milele.
5 Nyumba ninayokusudia kujenga itakuwa kubwa sana, kwani Mungu wetu ni mkuu zaidi ya miungu yote.
6 Lakini ni nani awezaye kumjengea nyumba ikiwa mbingu zenyewe hazimtoshi, wala mbingu za juu sana? Nami ni nani basi, hata nimjengee nyumba isipokuwa tu kama mahali pa kufukizia ubani mbele yake?