24 Hata ingawa jeshi la Shamu lilikuwa dogo, Mwenyezi-Mungu alilipa ushindi dhidi ya jeshi kubwa la watu wa Yuda kwa sababu hao watu wa Yuda walikuwa wamemwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao. Hivyo, Washamu wakatekeleza adhabu ya Mungu juu ya mfalme Yoashi.
25 Maadui walipoondoka, walimwacha akiwa amejeruhiwa vibaya sana, maofisa wake wakala njama wakamwulia kitandani mwake, kulipiza kisasi mauaji ya mwana wa kuhani Yehoyada. Alizikwa katika mji wa Daudi, lakini si kwenye makaburi ya wafalme.
26 Watu waliomfanyia njama walikuwa Zabadi mwana wa mwanamke Mwamoni jina lake Shimeathi, na Yehozabadi mwana wa mwanamke Mmoabu jina lake Shimrithi.
27 Habari za wanawe Yoashi za kuirekebisha nyumba ya Mwenyezi-Mungu na unabii wote juu yake, zimeandikwa katika Maelezo ya Kitabu cha Wafalme. Amazia mwanawe alitawala baada yake.