4 Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu kama baba yake.
5 Alimtumikia Mwenyezi-Mungu kwa uaminifu wakati wa kuishi kwa Zekaria, aliyemfundisha kumtii Mungu. Kadiri alivyomtafuta Mungu, Mungu alimfanikisha.
6 Uzia aliondoka akapiga vita dhidi ya Wafilisti, akazibomoa kuta za miji ya Gathi, Yabne na Ashdodi. Akajenga miji katika eneo la Ashdodi na kwingineko nchini Filistia.
7 Mungu alimsaidia kuwashinda Wafilisti, Waarabu waliokaa Gurbaali na Wameuni.
8 Waamoni walimlipa kodi, na sifa zake zikaenea hadi Misri, kwa sababu alipata nguvu.
9 Tena Uzia alijenga minara katika Yerusalemu penye Lango la Pembeni, Lango la Bondeni na Pembeni na kuiimarisha.
10 Hata nyikani pia alijenga minara, akachimba mabwawa mengi, maana alikuwa na mifugo mingi kwenye sehemu za miinuko na tambarare. Alikuwa na wakulima wa watunza mizabibu milimani, na katika ardhi yenye rutuba kwani alipenda kilimo.