1 Ahazi alianza kutawala akiwa na umri wa miaka ishirini; alitawala kwa muda wa miaka kumi na sita huko Yerusalemu. Yeye, hakufuata mfano mzuri wa Daudi babu yake, bali alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu,
2 na kufuata mienendo ya wafalme wa Israeli. Isitoshe, alitengeneza hata sanamu za kusubu za Mabaali,
3 akafukiza ubani kwenye Bonde la mwana wa Hinomu na kuwateketeza wanawe kama tambiko, akiiga desturi za kuchukiza za watu ambao walifukuzwa na Mwenyezi-Mungu wakati Waisraeli walipokuwa wanaingia nchini.
4 Alitoa tambiko na kufukiza ubani mahali pa kuabudia miungu mingine, vilimani na chini ya kila mti wenye majani mabichi.
5 Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, alimwacha mfalme Ahazi ashindwe na mfalme wa Aramu ambaye pia alichukua mateka watu wake wengi, akarudi nao Damasko. Kadhalika, alimfanya ashindwe na Peka, mwana wa Remalia, mfalme wa Israeli, ambaye alimshinda na kuua watu wengi sana.
6 Aliua askari mashujaa wa Yuda 120,000 katika siku moja. Ilitokea hivyo kwa sababu walimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao.
7 Zikri, askari mmoja shujaa wa Israeli, alimuua Maaseya, mwana wa mfalme, Azrikamu, kamanda wa Ikulu, na Elkana aliyekuwa mtu wa pili chini ya mfalme.