23 Watu wengi sana walikuja wakamletea Mwenyezi-Mungu tambiko huko Yerusalemu, pia wakamletea Hezekia, mfalme wa Yuda zawadi za thamani. Hivyo kutoka wakati huo, akasifiwa sana na mataifa mengine yote.
24 Wakati huo, Hezekia aliugua sana, karibu na kufa. Akamwomba Mwenyezi-Mungu, naye akamjibu na kumpa ishara.
25 Lakini Hezekia hakumtolea Mwenyezi-Mungu shukrani kwa hayo yote aliyomtendea kwa kuwa moyo wake ulikuwa umejaa majivuno. Hii ilisababisha kutaabika kwa Yuda na Yerusalemu.
26 Kwa hiyo ghadhabu ikawa juu yake, juu ya Yuda na juu ya Yerusalemu. Hatimaye Hezekia alinyenyekea akaacha kuwa na moyo uliojaa majivuno; yeye na wakazi wa Yerusalemu walijinyenyekesha kwa hiyo ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu haikuwajia wakati Hezekia alipokuwa hai.
27 Mfalme Hezekia alitajirika sana, akaheshimiwa. Alijitengenezea hazina za fedha, za dhahabu, za vito, za viungo, ngao na za aina zote za vyombo vya thamani kubwa.
28 Aidha, alijijengea mabohari ya kuhifadhia mazao ya nafaka, divai na mafuta, na mazizi kwa ajili ya ng'ombe na mengine kwa ajili ya kondoo.
29 Vivyo hivyo alijiongezea miji kwa ajili yake mwenyewe, makundi mengi ya ng'ombe na kondoo kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimkirimia mali nyingi.