4 Alijenga madhabahu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu mahali ambapo Mwenyezi-Mungu alikuwa amesema, “Jina langu litaabudiwa milele katika Yerusalemu.”
5 Alijenga madhabahu za kuabudia vitu vyote mbinguni kwenye nyua mbili za nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
6 Pia aliwatoa wanawe kama sadaka ya kuteketeza katika bonde la mwana wa Hinomu. Alipiga ramli, alibashiri na alitumia hirizi; hata alishirikiana na waaguzi wa mizimu na wachawi. Alitenda maovu mengi mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamkasirisha.
7 Nayo sanamu aliyoitengeneza, aliiweka katika nyumba ya Mungu mahali alipopazungumzia, mbele ya Daudi na Solomoni mwanawe: “Katika nyumba hii na katika Yerusalemu kati ya makabila kumi na mawili ya Israeli, ndipo mahali nitakapoabudiwa milele.
8 Na iwapo watu wa Israeli watajali kutenda yote niliyowaamuru, wakatii sheria zote, masharti, na maagizo yaliyotolewa kwa mkono wa Mose, basi kamwe sitawaacha wafukuzwe kutoka katika nchi hii ambayo niliwapa babu zao.”
9 Lakini Manase aliwapotosha watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu, wakatenda maovu zaidi kuliko mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyaangamiza mbele ya watu wa Israeli.
10 Mwenyezi-Mungu alimwonya Manase na watu wake, lakini hawakumsikia.