6 Mfalme Solomoni na mkutano wa Israeli wakakusanyika mbele ya sanduku la agano nao wakatoa sadaka za ng'ombe na kondoo wasiohesabika.
7 Kisha makuhani wakaliingiza sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu mahali pake, katika chumba cha ndani cha nyumba, mahali patakatifu sana, chini ya mabawa ya wale viumbe.
8 Hao viumbe wenye mabawa walitandaza mabawa yao juu ya mahali lilipowekwa sanduku, kwa hiyo sanduku na mipiko yake ya kulibebea vilikuwa chini ya mabawa.
9 Kwa kuwa mipiko hiyo ilikuwa mirefu sana, ncha zake ziliweza kuonekana kutoka mahali patakatifu mbele ya chumba cha ndani, lakini haikuweza kuonekana kutoka upande wa nje. Mipiko hiyo ingali mahali hapo hata leo.
10 Hakukuwa na kitu ndani ya sanduku la agano, ila vile vibao viwili vya mawe ambavyo Mose aliviweka humo kule Horebu, mahali Mwenyezi-Mungu alipofanya agano na watu wa Israeli, walipotoka Misri.
11 Ikawa makuhani walipotoka pale mahali patakatifu, (kwa sababu makuhani wote waliokuwapo bila kujali makundi yao, walikuwa wamejitakasa.),
12 Walawi wote waimbaji, wakiwamo Asafu, Hemani, na Yeduthuni, pamoja na Walawi wengine wa koo zao, wakiwa wamejivalia nguo zao za kitani safi huku wamebeba matoazi, vinanda na vinubi, walisimama upande wa mashariki wa madhabahu. Makuhani 120 wapiga tarumbeta walikuwa pamoja nao.