21 Sikia maombi yangu mimi mtumishi wako na ya watu wako Israeli wanapoomba wakielekea mahali hapa. Usikie maombi kutoka huko mbinguni na ukisha sikia, utusamehe.
22 “Mtu akimkosea mwenzake, naye akaletwa apate kuapa mbele ya madhabahu yako katika nyumba hii, na akiapa tafadhali
23 wewe usikie kutoka huko mbinguni, uchukue hatua na kuwahukumu watumishi wako. Aliye na hatia umwadhibu kadiri ya makosa yake; asiye na hatia umwachilie na kumpatia tuzo kadiri ya uadilifu wake.
24 “Wakati watu wako Israeli watakaposhindwa na maadui zao, kwa sababu ya dhambi walizotenda dhidi yako, nao wakitubu kwako na kukiri jina lako, wakiomba msamaha wako kwa unyenyekevu katika nyumba hii,
25 basi, usikie kutoka huko mbinguni. Usamehe dhambi zao na uwarudishe katika nchi uliyowapa wao na babu zao.
26 “Mvua isiponyesha kwa sababu wametenda dhambi dhidi yako, wakiomba wakielekea mahali hapa na kulikiri jina lako, pia wakiziacha dhambi zao, tafadhali
27 uwasikie kutoka huko mbinguni, na usamehe dhambi zao watumishi wako watu wako Waisraeli, huku ukiwafundisha kufuata njia nyofu, ukanyeshe mvua katika nchi yako hii ambayo uliwapa watu wako iwe mali yao.