12 Solomoni alimtolea Mwenyezi-Mungu tambiko za kuteketeza juu ya madhabahu aliyokuwa amemjengea Mwenyezi-Mungu mbele ya ukumbi wa hekalu.
13 Alitoa tambiko hizo kadiri ilivyotakiwa na amri ya Mose kila siku takatifu, yaani siku za Sabato, sikukuu za mwezi mwandamo, na sikukuu tatu za kila mwaka – sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, sikukuu ya majuma na sikukuu ya vibanda.
14 Akifuata maagizo ya Daudi baba yake, alipanga zamu za kila siku za makuhani na za Walawi waliowasaidia makuhani kusifu na kuzitekeleza kazi zao. Kadhalika aliwapanga walinda malango katika makundi aliyoyaweka kulinda kila lango; maana ndivyo alivyoamuru Daudi, mtu wa Mungu.
15 Nao hawakuyaacha maagizo mfalme aliyowaamuru makuhani na Walawi jambo lolote na kuhusu hazina.
16 Basi miradi yote ya Solomoni aliyofanya tangu jiwe la msingi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu lilipowekwa ilikamilika. Hivyo nyumba ya Mwenyezi-Mungu ilimalizika.
17 Kisha Solomoni alikwenda Esion-geberi na Elothi iliyo pwani mwa bahari, katika nchi ya Edomu.
18 Huramu alimpelekea merikebu zilizokuwa chini ya uongozi wa maofisa wake, pamoja na mabaharia stadi. Hao, pamoja na maofisa wa Solomoni, walisafiri hadi Ofiri, na kuchukua kutoka huko dhahabu, wakamletea mfalme Solomoni kiasi cha kilo 15,000.