12 Lakini jipe moyo! Tupigane kiume kwa ajili ya watu wetu na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; naye Mwenyezi-Mungu atutendee lile analoona ni jema kwake.”
13 Basi, Yoabu na watu wake walisonga mbele kwenda kupigana na Waaramu, nao Waaramu walikimbia.
14 Waamoni walipoona kuwa Waaramu wamekimbia, nao pia walimkimbia Abishai na kuingia mjini. Yoabu akaacha kupigana na Waamoni, akarudi Yerusalemu.
15 Lakini Waaramu walipoona kwamba wameshindwa na Waisraeli, walijikusanya pamoja.
16 Hadadezeri aliagiza Waaramu waliokuwa ngambo ya mto Eufrate waletwe, wapelekwe huko Helamu wakiongozwa na Shobaki kamanda wa jeshi la Hadadezeri.
17 Daudi alipopata habari, aliwakusanya pamoja Waisraeli wote, akavuka mto Yordani na kwenda mpaka Helamu. Nao Waaramu walijipanga tayari kwa vita dhidi ya Daudi, wakaanza kupigana naye.
18 Lakini Waaramu walikimbia mbele ya Waisraeli. Daudi aliwaua Waaramu 700 waliokuwa madereva wa magari ya vita, wapandafarasi 40,000. Pia alimwumiza Shobaki kamanda wa jeshi lao, naye akafia papo hapo.