20 Yoabu alifanya hivyo ili kubadilisha mambo. Lakini, wewe bwana wangu, una hekima kama ya malaika wa Mungu hata unaweza kujua mambo yote yaliyoko duniani.”
21 Kisha, mfalme akamwambia Yoabu, “Sasa sikiliza, natoa kibali changu ili umrudishe nyumbani yule kijana Absalomu.”
22 Yoabu alianguka chini kifudifudi, akasujudu na kumtakia mfalme baraka, akasema, “Leo, mimi mtumishi wako, bwana wangu mfalme, ninajua kuwa nimepata kibali mbele yako, kwa kulikubali ombi langu.”
23 Hivyo, Yoabu aliondoka, akaenda Geshuri kumleta Absalomu mjini Yerusalemu.
24 Lakini mfalme akasema, “Absalomu aishi mbali nami; aishi nyumbani kwake. Asije hapa kuniona.” Hivyo, Absalomu akawa anaishi mbali, nyumbani kwake na hakumwona mfalme Daudi.
25 Katika Israeli yote, hakuna yeyote aliyesifiwa kwa uzuri kama Absalomu. Tangu nyayo zake hadi utosini mwake, Absalomu hakuwa na kasoro yoyote.
26 Kila alipokata nywele zake, (na kila mwishoni mwa mwaka alikata nywele zake kwani zilikuwa nzito), alipozipima, zilikuwa na uzito wa kilo mbili kulingana na vipimo vya kifalme.