8 Abneri mwana wa Neri, kamanda wa jeshi la Shauli alikuwa amemchukua Ishboshethi mwana wa Shauli na kumpeleka huko Mahanaimu.
9 Huko, Abneri akamtawaza Ishboshethi kuwa mfalme wa nchi ya Gileadi, Ashuru, Yezreeli, Efraimu na Benyamini na Israeli yote.
10 Ishboshethi alikuwa na umri wa miaka arubaini alipoanza kuitawala Israeli, naye alitawala kwa muda wa miaka miwili. Lakini kabila la Yuda lilimfuata Daudi.
11 Daudi alikuwa mfalme wa kabila la Yuda kwa muda wa miaka saba na nusu, makao yake yalikuwa huko Hebroni.
12 Abneri mwana wa Neri, pamoja na maofisa wa Ishboshethi, mwana wa Shauli, waliondoka Mahanaimu na kwenda Gibeoni.
13 Yoabu mwana wa Seruya na watumishi wengine wa Daudi, nao walitoka na kukutana na Abneri na watu aliokuwa nao kwenye bwawa lililoko huko Gibeoni. Kikosi kimoja upande mmoja wa bwawa na kingine upande mwingine.
14 Abneri akamwambia Yoabu, “Waruhusu vijana wapambane mbele yetu!” Yoabu akamjibu, “Sawa.”