6 Daudi akamwambia Abishai, “Sasa, Sheba mwana wa Bikri, atatuletea madhara kuliko Absalomu. Chukua watumishi wangu, umfuatie Sheba asije akaingia kwenye miji yenye ngome akaponyoka, tusimwone tena.”
7 Abishai akatoka akiwa pamoja na Yoabu, Wakerethi na Wapelethi pamoja na mashujaa wote. Hao wote waliondoka Yerusalemu kwenda kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.
8 Walipofika kwenye jiwe kubwa lililoko huko Gibeoni, Amasa akatoka kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa vazi la kijeshi, na ndani ya vazi hilo kulikuwa na mkanda ulioshikilia upanga kiunoni mwake ukiwa kwenye ala yake. Yoabu alipokuwa anakaribia, upanga wake ulichomoka alani ukaanguka chini.
9 Yoabu akamwambia Amasa, “Je, hujambo ndugu yangu?” Yoabu akamshika Amasa kidevuni kwa mkono wa kulia kana kwamba anataka kumbusu.
10 Lakini Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu. Basi, Yoabu akamchoma Amasa upanga tumboni, matumbo yake yakatoka nje, akafa. Yoabu hakumchoma upanga mara mbili.Kisha, Yoabu na nduguye Abishai wakaendelea kumfuatilia Sheba mwana wa Bikri.
11 Mtu mmoja wa Yoabu akaja akasimama karibu na mwili wa Amasa, akasema, “Yeyote anayempenda Yoabu na yeyote anayempenda Daudi, na amfuate Yoabu!”
12 Amasa alikuwa bado anagagaa kwenye damu yake katikati ya barabara kuu. Kwa hiyo, kila mtu aliyepita hapo, alipomwona, alisimama. Lakini yule mtu alipoona kwamba watu wote walikuja na kusimama hapo, aliuondoa mwili wa Amasa barabarani, akaupeleka shambani na kuufunika kwa nguo.