26 Wale wanaokula pamoja naye, ndio watakaomwangamiza. Watamwangamiza na jeshi lake litafagiliwa mbali na wengi watauawa.
27 Hapo wafalme hao wawili wataketi pamoja mezani kula, lakini kila mmoja anamwazia mwenzake uovu, na kudanganyana. Ila hawatafanikiwa, maana wakati uliopangwa utakuwa bado haujatimia.
28 Mfalme wa kaskazini atarudi nchini mwake akiwa na mali nyingi, lakini nia yake moyoni ni kulitangua agano takatifu. Atafanya apendavyo, kisha atarudi katika nchi yake.
29 “ ‘Katika wakati uliopangwa ataivamia nchi ya kusini kwa mara nyingine, lakini safari hii, mambo yatakuwa tofauti.
30 Meli kutoka Kitimu zitamshambulia, naye atashikwa na hofu. Kisha atarudi nyuma huku amejaa hasira na atalitangua agano takatifu. Hapo atafuata shauri la wale walioasi agano takatifu.
31 Wanajeshi wake watalitia najisi hekalu na ngome zake, watakomesha tambiko za kuteketezwa kila siku na kusimamisha huko hekaluni chukizo haribifu.
32 Atawashawishi kwa hila wale walioasi agano, lakini watu walio waaminifu kwa Mungu wao watasimama imara na kuchukua hatua.