38 Badala ya miungu hiyo atamheshimu mungu mlinzi wa ngome, ambaye wazee wake kamwe hawakumwabudu, atamtolea dhahabu, fedha na vito vya thamani, na zawadi za thamana kubwa.
39 Atazishughulikia ngome zake kwa msaada wa mungu wa kigeni. Wale wanaomtambua kuwa mfalme, atawatunukia heshima kubwa, atawapa vyeo vikubwa na kuwagawia ardhi kama zawadi.
40 “ ‘Wakati wa mwisho mfalme wa kusini atamshambulia mfalme huyo wa kaskazini. Lakini mfalme wa kaskazini atajibu mashambulio hayo kwa nguvu kama kimbunga, akitumia magari ya farasi, wapandafarasi na meli nyingi. Atazivamia nchi nyingi na kupita katika nchi hizo kama mafuriko ya maji.
41 Ataivamia hata nchi ile tukufu na kuua maelfu ya watu. Lakini nchi za Edomu, Moabu na sehemu kubwa ya Amoni, zitaokoka kutoka mikononi mwake.
42 Wakati atakapozivamia nchi hizo, hata nchi ya Misri haitanusurika.
43 Atamiliki hazina za dhahabu, fedha na vito vyote vya thamani vya nchi ya Misri. Watu wa Libia na watu wa Kushi watafuata nyayo zake.
44 Lakini habari kutoka mashariki na kaskazini zitamtisha. Naye atatoka kwa hasira kubwa ili kukatilia mbali na kuangamiza wengi.