8 Baadaye, akaja Danieli, anayeitwa pia Belteshaza, jina la mungu wangu, ambaye roho ya miungu mitakatifu imo ndani yake. Nami nikamsimulia ndoto yangu, nikasema:
9 Ee Belteshaza, uliye mkuu wa waganga, nafahamu kuwa roho ya miungu mitakatifu imo ndani yako, na kwamba hakuna fumbo lililo gumu kwako. Hii ndiyo ndoto yangu; niambie maana yake.
10 “Nilipokuwa nimelala, niliona maono haya: Niliona mti mrefu sana katikati ya dunia.
11 Mti uliendelea kukua, ukawa imara na kilele chake kikafika mbinguni. Uliweza kuonekana kutoka kila mahali duniani.
12 Majani yake yalikuwa mazuri. Ulikuwa umejaa matunda, kiasi cha kuitosheleza dunia nzima. Wanyama wote wa porini walipata kivuli chini yake, na ndege wa angani walikaa katika matawi yake. Viumbe vyote vilipata chakula kutoka mti huo.
13 “Nilipokuwa nimelala kitandani, niliona maono: Mlinzi mtakatifu alishuka kutoka mbinguni.
14 Akapaaza sauti akisema, ‘Kateni mti huu na kuyakatakata matawi yake. Pukuteni majani yake na kuyatawanya matunda yake. Wanyama na watoroke chini yake na ndege kutoka matawi yake.