11 Waisraeli wote wameiasi sheria yako, wamekuacha wakakataa kukutii. Kwa sababu tumekukosea, tumemwagiwa laana na viapo vilivyoandikwa katika sheria ya Mose, mtumishi wako.
12 Umethibitisha yale uliyosema utatutenda sisi pamoja na watawala wetu kwa kuuadhibu mji wa Yerusalemu vikali zaidi ya mji mwingine wowote duniani.
13 Umetuadhibu kama ilivyoandikwa katika sheria ya Mose, lakini mpaka sasa, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, hatukuomba msamaha wako kwa kuziacha dhambi zetu na kutafakari uaminifu wako.
14 Kwa hiyo, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ulikuwa tayari kutuadhibu, na ukafanya hivyo, kwa kuwa daima unafanya yaliyo ya haki, nasi hatukukusikiliza.
15 “Na sasa ee Bwana, Mungu wetu, uliyewatoa watu wako nchini Misri kwa nguvu yako kuu na kulifanya jina lako litukuke mpaka sasa, tunasema kwamba tumetenda dhambi; tumefanya maovu.
16 Ee Bwana, kwa kadiri ya matendo yako ya haki usiukasirikie wala kuughadhibikia mji wako wa Yerusalemu, mlima wako mtakatifu. Watu wote wa nchi za jirani wanaudharau mji wa Yerusalemu na watu wako, kwa sababu ya dhambi zetu na maovu waliyotenda wazee wetu.
17 Kwa hiyo, ee Mungu, isikilize sala yangu na maombi yangu mimi mtumishi wako. Kwa hisani yako, uifadhili tena maskani yako iliyoharibiwa.